Umuhimu Wa Ubatizo
Warumi 6:1-23
Wageni wetu karibuni sana. Leo Tunaendelea na Seminar yetu kuhusu HAKI IPATIKANAYO kwa njia ya Imani. Na hapa Paulo anafungua sura hii kwa kuuliza swali: Je tudumu dhambini ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha kwani Neema imekuja ili kutuokoa kutoka dhambini na sio ili tuendelee kuishi katika dhambi. Tunapompokea Yesu kwa kujisalimisha kwake na kujikana nafsi na hivyo kuifia dhambi.
🎚️Tukiisha kufa, tunazika utu wetu na Yesu sasa anakuwa ndie Mungu wetu, tunakuwa tumeifia nafsi na hivyo kuifia dhambi. Tukiisha kufa, tunazika utu wetu wa kale kwa njia ya ubatizo, kama kielelezo cha kufa na kuzikwa Pamoja na Kristo na hivyo tunaungana naye na kuwa mali yake.
🎚️Lakini Kristo hakubakia kaburini, alifufuka katika utukufu; vivyo hivyo tunapokuwa tumezikwa ktk maji ya ubatizo tunatoka tukiwa tumekamilisha hatua alizozisema Yesu, kwamba ili tuupate ufalme wa mbinguni hatuna budi kuzaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho.
🎚️Kwa kuwa sasa tunakuwa viumbe vipya, tunapaswa kuenenda katika upya wa uzima, yaani kuishi maisha mapya ya utii katika Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Mwili wa dhambi au utu wa kale wa dhambi unakuwa umekufa na kubatilika, na hivyo hatupaswi kutumikia nafsi au dhambi tena. Tunakuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu.
🎚️Lakini hili litadumishwa tu kwa kumruhusu Kristo aishi na kutawala daima ndani yetu. Ukubali wetu kumruhusu Kristo atawale moyoni daima ni jambo la muhimu sana linalopasa kufanyika kila wakati.
🎚️Hivyo tunajitoa kumtumikia Mungu, kwa kumtii na kufanya mapenzi yake. Kudai tu kwamba tunamtumikia Mungu huku tukivunja moja ya maagizo yake tunaonyesha kwamba bado tuna Mungu mwingine aitwaye NAFSI ambae ana uadui na Mungu wa kweli aliye Muumbaji.
🎚️Yesu aliuliza swali “Na kwanini mnaniita Bwana Bwana walakini hamyatendi nisemayo? Luka 6:46 matokeo yake mwishoni ni kuanguka tu. Aya ya 49 pitia pia Mathayo 7:21-23. Imani ya kweli inayopelekea utii kwa Mungu ndiyo pekee itakayosimama hadi mwisho aya ya 47-48
🎚️Tunapokuwa tumeokolewa kwa Neema, hatuwi tena chini ya sheria, bali chini ya Neema. Kuwa chini ya Neema ni kusamehewa dhambi na kuvikwa haki ya Kristo. Ni kuenenda kwa Roho kwa njia ya Imani. Wagalatia 5:18 inasema “Lakini mkiongozwa na Roho hamuwi chini ya Sheria” na Bwana Yesu alisema kuwa Roho Mtakatifu atatuongoza atutie kwenye kweli yote, kwa hiyo tunapoongozwa na Roho wa Mungu tutaongozwa kumtii yeye. Yohana 16:13
Bwana akubariki sana🙌
📚📚📚📚📚📚📚📚
0 Comments