2⃣ *SEMINA YA NENO LA MUNGU KWA WATU WOTE - MOSHI - UWANJA WA MPIRA MAJENGO

 Na MWL. CHRISTOPHER MWAKASEGE*

SOMO: NAMNA YA KUSHINDA VIKWAZO VINAVYOZUIA USIFIKIE MALENGO YAKO KIMAISHA.

*TAREHE:  26 /02/ 2019

*SIKU YA PILI*



SEHEMU YA KWANZA

*UTANGULIZI*
Leo ikiwa ni siku yetu ya pili na somo  letu lina kichwa kinachosema *NAMNA YA KUSHINDA VIKWAZO VINAVYOZUIA USIFIKIE MALENGO YAKO KIMAISHA.*

Jana tuliangalia kikwazo cha kwanza ni *AKILI KUFUNGWA NA SHETANI* na tukaangalia kwenye kile kitabu cha *Luka 8:26 - 39* tukaangalia kwa undani pamoja na mistari mingine na maelezo kwa undani.

Saa nyingine huwa nawaza sana  namna akili ya mwanadamu ilivyo na ambavyo inafanya mambo makubwa je kama tusingepita kwenye dhambi ingekuwaje? Kwa sababu vitu vingi vimebuniwa na akili ya mwanadamu ambayo iko kwenye dhambi na ina kiwango cha kufanya kitu ilichokifanya, sasa fikiria kama asingekuwa na dhambi ingefanya vikubwa kiasi gani? Sijasoma kwenye Biblia, lakini najaribu kufikiria kuwa kama tukifika mbinguni halafu Mungu atatuonyesha tumetumia kiwango gani cha akili zetu alizotupa na tukajikuta tumetumia kiasi kidogo sana mfano ¼, au 5% au 10% na asilimia iliyobaki akatuonyesha kulikuwa na kitu gani .Pia hiyo akili ambayo haijatumika  je tungeitumia tungekuwa na maisha ya aina gani. Nakuambia watu wengi wangekata rufaa ya kurudi duniani kwa sababu ndani yake wangegundua kuwa kuna vitu vikubwa sana.

Tukiangalia mfano wa Yusufu  mtoto wa mzee Yakobo kwenye Mwanzo 41, aliitwa ofisini kwa Farao kutafsiri ndoto ya Farao aliyoiota usiku na kurudia mara mbili. Mara ya kwanza Farao aliota ng'ombe wanono saba halafu wakaja wengine waliokonda kutoka kwenye mto. Wale waliokonda wakawala wale wenye afya na hata baada ya kuwala wakabaki wamekonda vile vile, akaamka; akalala na kuota ndoto nyingine akaona masuke na asubuhi yake akatafuta msaada wa tafsiri kila kona kwa waganga, wachawi na wenye hekima ili wamsaidie.

Mpaka mfanyakazi wake akaeleza alivyokutana na Yusufu jela na namna alivyo weza kuwatafsiria ndoto zao. Baada ya kusikia habari ya Yusufu ndipo Farao akaagizwa Yusufu aitwe mbele zake.Yusufu alipopewa taarifa za kuitwa kwa Farao tunona akamtafsiria Farao ndoto zake na kumweleza juu ya ujio wa miaka 7 ya chakula na unono. Baada ya pale Farao akata kujua zaidi miaka 7 ya njaa. Aliambiwa hiyo njaa itakuwa kubwa mno kiasi ambacho miaka 7 ya unono itaonekana kama haikuwepo ndio maana aliona ng'ombe waliokonda wakiwala walionona. Baada ya kuwala wale ng’ombe , wale waliokonda  hawakunenepa ili kuonyesha kuwa kipindi cha njaa kitakuwa kibaya sana.

Yusufu alipomaliza kumtafsiria Farao ndoto alimwelezea kitu cha kufanya kwa sababu alikuwa anajiandaa kurudi jela. Alimwambia Farao “tafuta mtu mwenye akili na hekima umweke kwenye nafasi afanye yafuatayo

*Mwanzo 41:33 - 36*
_“Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.”_

Alipomaliza kusema hivyo Farao akasema
*Mwanzo 41:38 - 40*
_“Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”_

Mtu aliyekuwa anatakiwa kwenye hii nafasi alitakiwa awe ana akili ya miaka 14 kusaidia Misri na nchi za jirani. Alitakiwa awe ana hekima pamoja na Roho wa Mungu ili kuweza kukamilisha jukumu hilo. Yusufu aligundua kuna kitu Farao alitakiwa akitolee nafasi (position) kwa sababu anaweza patikana mtu mwenye akili lakini asiwe na  mahali pa kutumia akili zake.

Kuna watu wana a

kili lakini hawana hekima na wengine wana hekima akili hawana. Yusufu alikuwa na hivyo vyote  pia alikuwa na Roho wa Mungu ndani yake. Kwa maana hiyo Mungu alimpa nafasi ili aweze tumia akili, hekima na Roho ya Mungu  iliyokuwa ndani yake katika kufanya alichotakiwa kufanya kwa miaka 14.

Mwanzoni kabisa Yusufu aliotea ndoto akiwa na miaka 17 lakini alipewa kuwa waziri mkuu akiwa na miaka 30, kwa hiyo miaka 13 ilimtesa kufukia mahali pa kuweza kutumika miaka 14. Kwa sababu alipitia wakati mgumu sana miaka hiyo 13 maana  Mungu alimleta duniani kwa kazi hizo kubwa. Moja ya kazi ni kuhakikisha ile miaka 14 pale Misri akili zake zinatumika sawasawa kwa sababu alisema

*Mwanzo 45:7 - 8*
_“Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri.”_

Maana yake amekuwa na akili iliyomfanya kuwa baba kwa Farao mahali ambapo kwa jinsi ya kawaida isingewezekana pia akawa baba kwa taifa la Misri na kwa ndugu zake. Yusufu ndoto (vision) yake ilikuwa ya contract ya miaka 14. Lakini alifanya vizuri kiasi ambacho hakustaafishwa baada ya muda wake kuisha bali aliendelea na kazi mpaka alipo kufa.

Kumbuka Yusufu alipewa akili ya kusaidia ndugu zake lakini ndugu zake walimkataa hata alipoenda kuwapelekea chakula walipomwona walimkasirikia wakaanza kupanga kumu ua. Sasa fikiria walitaka kuua akili ya namna gani kwa kubebeshwa kitu cha aina gani. Kwa hiyo ili wasimuue wakakubaliana kumtumbukiza kwenye kisima kisicho na maji halafu wakafikiria tena kuwa wamuuze kama mtumwa bila kujua thamani ya akili iliyokuwa inauzwa.

Waishmaeli nao wakaja kumuuza kwa Potifa na Potifa baadae akamtazama akagundua Yusufu ana baraka fulani na sio akili tu. Potifa akamweka Yusufu kuwa  kiongozi wa kila kitu nyumbani kwake. Aliposhindwana na mke wa Potifa akaishia jela, sasa fikiria ni akili gani ambayo ilikuwa imefungwa jela. Kuna wengine wamefungwa jela (jela hizi za kawaida kwa makosa halali au kwa kusingiziwa/kuonewa) na wana akili kama ya Yusufu.

Pia mkuu wa jela akagundua baraka zilizokuwa juu ya Yusufu na kumpa cheo. Naye Yusufu akamsaidia mtu mkubwa sana katika taifa la Misri kwa kumtafsiria ndoto yake na akamwambia akirudi kazini kwake  amkumbuke ili aweze toka jela. Lakini yule mtu alimsahau kwa hiyo Yusufu  alisahauliwa jela miaka miwili.

Ninaposoma hizi habari huwa namshangaa sana Mungu. Inawezekana umesahauliwa huna nafasi yoyote, huna kazi lakini hujui akili uliyobeba na inawezekana hata waliokuzunguka hawajui akili uliyobeba.Maana unaweza ukawa na upako lakini kuna watu wanaojaribu kutafuta kukuua na Mungu amenyamaza. Unaweza ukawa ndani ya birika na ndugu zako wakakuchukia kabisa. Usije ukafikiri Mungu amekuacha maana nguvu za Mungu ziko pamoja na wewe. Inawezekana unaishi maisha kama ya kitumwa lakini mkono wa Bwana uko pamoja na wewe.

Yusufu alikuwa na Mungu kwenye kila mazingira toka anauzwa, alipopelekwa mahakamani kwa sababu ya mke wa Potifa Mungu alikuwa pamija nae. Alipokuwa jela alikuwa pamoja na  Mungu  kwa hiyo kila sehemu Mungu alikuwa pamoja nae. Kwa hiyo usije ukafikiri waliofungwa jela hawana Mungu wako pamoja na Bwana.
Shetani alikuwa anagombana na akili za Yusufu ili  zisipate nafasi ya kutumika maana alikuwa ana akili ya kusaidia familia yake lakini alinyimwa heshima nyumbani kwake. Akili alilozokuwa nazo Yusufu zilikuwa na uwezo wa kumsaidia baba yake lakini aliondolewa nyumbani kwao na kukatiwa mawasailiano na baba yake ili ajue kwamba amekufa. Shetani alikuwa  akiwinda baba yake yaani mzee Yakobo asipate  msaada wa akili za Yusufu.
Unaweza ukawa unafurahia biashara uliyonayo na kufikiri kwamba umefika lakini Mungu ana kitu kikubwa kuliko unachofikiri. Ila hujajua kwamba huko ndani yako kuna kitu gani kimekaa na kwanini ndani yako unaona ndoto kubwa au unaona hujaridhika mahali ulipo kumbe Mungu anajaribu kukusukuma kukuonyesha kwamba ndani yako amekuwekea kitu kikubwa kuliko unacho fikiri. Hivyo usitosheke na mahali ulipo kisukume

na usonge mbele na ukimwendea Mungu atakuonesha mahali unapotakiwa kuwa.
Mungu alimpa Yusufu miaka 14 ya kutumia zile akili. Na ndiyo maana si suala la kuishi maisha marefu ni suala la kuishi katika mapenzi ya Mungu. Kuna wengine wanaishi maisha marefu na maisha yao hutaki hata kuyasikia, maana ni hasara tu mpaka kwa udongo. Lakini kuna wengine wana maisha mafupi kama ya Yesu, maana yeye alikufa kabla ya kufikisha miaka 40 na ni miaka 3 ndiyo iliyomleta hapa duniani miaka mingine unaona wakiandika habari zake kwa uchache sana. Miaka yake 3 ilibadilisha kila kitu na kuweka alama ambayo shetani hawezi kufuta.
Sijajua Mungu amekupa mtu wa namna gani, au kwamba Mungu amekubebesha akili za namna gani ila ninachojua akina Yusufu wako tena yawezekana ni wewe. Wakati ukifika haijalishi uko jela au umesingiziwa Mungu atakutoa tu huko, ikifika saa ya kwako Mungu atatengeneza njia tu hata kama hakuna njia na kukufikisha mahali kila mtu atakutazama na kusema kama si Mungu aliyekuwa pamoja naye huyu mtu na aseme sasa.
Na ndiyo maana Yusufu pamoja na kulia alipowaona ndugu zake hakuwa na sababu ya kuwachukia na kuwakasirikia alijua ya kwamba kama si Mungu wasinge fika pale na yeye asingefika pale. Kwa hiyo ukiona watu wanakuchukia na kukupiga vita njiani wakati unasonga mbele huhitaji kuwakasirikia wewe songa mbele maana hao hao wanaokuchukia leo kesho watakuja kukuomba mkate.
Kwa hiyo ukiwa na akili kubwa usishindane na vidogo. Usiwe na muda wa kupoteza kwenye vitu ambavyo vinakuletea hasara tu.
Nilikuambia *akili sio ubongo* akili iko ndani ya nafsi na ubongo uko ndani ya mwili lakini Mungu aliviumba vifanye kazi kwa pamoja kwa kushirikiana.
*Ayubu 32:8*
_“Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.”_

*Mwanzo 2:7*
_“Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”_

Hivyo pumzi ilitumika kuweka nafsi na pumzi ilitumika kuweka akili kwa hiyo akili iko ndani ya nafsi na ubongo ni kiungo cha mwili kilichopo kwenye kichwa na Mungu ameweka vyote hivi vifanye kazi kwa pamoja

*MIFANO MICHACHE AKILI ZINAPOFANYA KAZI NA UBONGO VIZURI:-*

MFANO WA KWANZA
*I. UBONGO UTAKUSAIDIA KUPOKEA ELIMU AKILI ITAGEUZA ELIMU ULIYOPATA KUWA MAARIFA.*

Elimu haikupi maisha; inaweza kukupa kazi, cheo au pesa lakini si maisha bali maarifa ndiyo yakupayo maisha.Ni muhimu sana kuzungumza na watoto jambo hili kwa sababu kisomo ambacho hakiwezi kugeuka kuwa maarifa maana hakina msaada kwao maana Biblia inasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa na si kwa kukosa elimu. Ubongo hauwezi kutengeneza maarifa maana haukuumbiwa kutengeneza maarifa.

Watu wengi sana wanafikiria kumaliza shule wapate kazi, jiulize baada ya kupata kazi nini kinafuata? Maana wapo wengi sana wana kazi lakini hawana maisha kwa sababu akili zao hazijapata nafasi ya kufanya kazi na ubongo wao.

MFANO WA PILI
*II. UBONGO UNAKUPA NAFASI YA KUPOKEA HABARI LAKINI AKILI NDIZO ZINAZOWEZA KUGEIUZA HIZO HABARI KUKUPA UFAHAMU .*

Maana kazi ya vyombo vya habari si kukuhabarisha tu bali na kukufahamisha. Kwa hiyo kama hupati ufahamu kwenye hizo habari maana yake umesoma tu lakini hujapata cha zaidi, yaani ubongo umekusaidia kuangalia na kusikiliza lakini akili hazikuwa mahali hapo.


MFANO WA TATU
*III. UBONGO UNAONA MATATIZO AKILI INAONA FURSA KWENYE HAYO MATATIZO.*

*1 Mambo ya Nyakati 12:32*
_“Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.”_

Nataka uone hapa anaposema walikuwa *watu wenye akili za kujua nyakati na kitu cha kufanya kwenye nyakati* Kwanini? Kwa sababu ukisoma kile kitabu cha Mhubiri;

*Mhubiri 3:1-2*
_“Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa;”_
Mungu alipanga vitu viende kwa muda na katika huo muda kuna vitu ambavyo tunatakiwa kufanya.
*MFANO*
Mungu alipomuumba mwanadamu pamoja na umuhimu wa magari hakutuumbia magari, na kwa sababu hiyo

mwanadamu alipozaliwa na kuanza kutembea huku duniani kukosekana kwa barabara hakukuwa tatizo la kimaendeleo kwa nyakati zile, ubongo ulikuwa unaona kabisa kwamba hakuna barabara na akili ilikuwa inasema huna shida nayo. Lakini ikafika mahali muda unadai vitu viende kwa speed ndipo maswali ya usafiri yakaanza kuja na ndipo vikaja vyombo vya usafiri ili kurahisisha usafirishaji na mawasiliano na kurahisisha maendeleo kwenda kwa haraka. Sasa ilipofika mahali pa namna hiyo ubongo unapoona magari halafu hauoni barabara basi wenyewe (ubongo) unasema hili ni tatizo akili inasema hii ni fursa.

Kwa hiyo ukitumia ubongo bila kutumia akili utalalamika.Ukitumia ubongo na akili utatafuta majibu ya changamoto na tatizo hilo.

Ukiumwa jino kwako wewe unayeumwa jino ni tatizo lakini kwa daktari ni fursa. Ukiona garage zinajengwa wameona magari yanaharibika au wanatafuta fursa. Kama akili ikiwa kazini tafsiri ya vitu vilivyoko kwenye nyakati zilizoko zinakuwa tofauti kufuatana na nyakati. Ndio maana Mungu aliwaweka wana wa isakari wenye kujua nyakati na mambo yanayotakiwa yafanyike kwenye hizo nyakati nao walikuwa 200 na walikuwa viongozi wa ndugu zao. Mtu anayeweza kufikiri kesho yako kabla kesho haijafika uwe na uhakika atakuwa kiongozi wako. Mvua inanyesha unatafuta mwamvuli zamani hakukuweko miamvuli, mvua inanyesha unatafuta mwamvuli zamani tulikuwa tunatumia majani ya migomba lakini kuna mtu akafikiri akaona jinsi ambavyo mvua ikiisha unavyohangaika kutupa lile jani akafikiri kitu cha kujifunika ili mvua ikiisha anajifunika na kila alichofikiri unakilipia.

Mungu alijua kabisa ili mwanadamu aweze kuishi vizuri anahitaji masaa 8 kati ya 24 na ukilimbikiza madeni ya usingizi utakuta unakosa utulivu na macho yanashindwa kuangalia vizuri, baada ya muda utaanza kupata shida ya kula chakula, sasa kama usingizi ulikuwa wa muhimu namna hii kwanini Mungu hakutengeneza kitanda! Na ukiangalia ⅓ ya maisha ya Mwanadamu anatumia kitandani kwa hiyo hii inamaanisha ni sehemu muhimu sana. Kwanini Mungu alipotuumba asingetengeneza na kitanda ni kwa sababu alitupa akili kwamba tuamue tunalala chini au tunatengeneza kitanda ni juu yetu.

Tulienda hoteli moja kule Washington DC na tulikuwa kwenye msafara wa viongozi fulani miaka kadhaa iliyopita tukapewa chumba. Tukakitazama kile chumba na kitanda chake na tukakuta vitu vimewekwa pale mezani kwa hiyo tukaamua kuvisoma tukashangaa kumbe ni button za kukusaidia unataka kulalaje! Kwetu ukitaka kulala kichwa juu unaweka mto ukitaka kulala flat unaondoa mto wenzetu wameondoa hiyo shida ni unabonyeza tu button na kitanda kina ji adjust chenyewe. Lakini uliza bei ya chumba! Ni ghali mnoo.

Nilienda Canada wakati wa baridi  na nilipolalamika kuna baridi wakanipeleka kwenye chumba na chumba wameki balance hali ya joto na kuna blanket linatumia umeme. Nikaona amenyanyua blanket akavuta wire akaenda kwenye soketi ya umeme akachomeka halafu akawasha umeme halafu akaniambia ingia hapo ulale nikakataa! Walipoona nimeshtuka namna hiyo yule mwenyeji wangu akaingia akajaribu akaniambia si unaona mimi sijapata shock hamna shida! nikamwambia  aaa wapi! Sasa katika shida yote ile walitafuta kurahisisha maisha akili na ndio maana akili zao zimeingia kazini. Wakati wewe unalalamika baridi wao wanaishi kwa sababu akili zao zinafanya kazi. Mahali wewe unalalamika wenzio wanajikita katika kutafuta fursa.

Wageni wengi sana wanakuja katika nchi hii kwa sababu ya shida tulizo nazo, wameona fursa  sasa kama wameona fursa waulize wameonaje ili na wewe utumie hizo fursa.

*MFANO WA NNE*
*IV. UBONGO UNAJIANDAA KUFANYA HARUSI LAKINI AKILI INATENGENEZA NDOA*

*1Petro 3:7*
_Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe_


Biblia haisemi wanaume tukae na wake zetu kiroho, kwa hiyo usijaribu kukaa na mke wako kiroho, kaa nae kwa akili. Ndani ya akili hizo Mungu atakupa neema ya kumsaidia kumpa heshima anayostahili. Lakini kuona ile nafasi kwa jinsi ya mwili ni chombo kisichokuwa na nguvu lakini katika ulimwengu wa roho wana nguvu kuliko sisi!  Kwanini _Mungu ameumba jambo jipya mwanamke atamlinda mwanaume_ wanawake ni walinzi wazuri sana katika ulimwengu wa roho, wana nguvu za kiroho kuliko wanaume lakini inapokuja kwenye maisha ya kawaida Biblia inasema mpe heshima maana ni kiumbe dhaifu.

Unaweza ukampenda mke wako lakini usimheshimu, Biblia inasema kama warithi pamoja wa neema,je huwa unamshirikisha mke wako kwa kiwango gani kitu ulichonacho? Kuna watu ambao vitu vyao ni siri kiasi kwamba hata akifa ni shida kujua hata alikuwa na account wapi, alikuwa pesa kiasi gani, viwanja vingapi! Hata mke hajui na siku akifa anaanza kuhangaika kama mtu mwingine.

*Tito 2:3-5*
_Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe._


Biblia inatuambia wanawake watu wazima wamepita mahali wameona umuhimu wa akili ndio maana biblia inasema wasaidieni hawa wanawake vijana watieni akili.Mwanamke anatumia akili kumpenda mume wake na mwanaume anatumia akili kumpa heshima mke wake. Hapo roho haitajwi katika kupenda wala kumpa mke heshima bali ni akili inatumika.

Biblia inasema na kuwapenda watoto wao, maana unaweza ukawapenda watoto yatima lakini wa kwako usiwapende.Haitoshi tu kusema unawapenda watoto maana unaweza ukasahau kuwapenda watoto wako mwenyewe. Ndio maana biblia inasema wanawake wawatie wanawake vijana akili za kuwapenda watoto wao na waume zao, kuwa wenye kiasi, na kuwa safi. Kwa hiyo mwanamke akiwa mchafu shida ni akili zake. Kwa hiyo kama pepo limemfanya kuwa mchafu ina maana limeshika akili zake, maana  inatakiwa akili zitumike ili kumfanya kuwa safi.

Mwanamke anatakiwa kufanya kazi nyumbani mwake.  Maana anaweza fanya kazi kwingine lakini nyumbani mwake asifanye kazi. Pia wanawake wanatakiwa kuwa wema na kuwatii waume zao wenyewe. Kuna baadhi wanawake wanawatii sana wachungaji zao kuliko waume zao, maana si vibaya kumtii mchungaji. Lakini kumbuka mume akimfukuza huyo mke wake, mchungaji hawezi kumuoa. Pia mke wa mchungaji nae akikaa vizuri kwenye nafasi yake endapo akienda mwanamke aliyefukuzwa na mume wake akaenda kwa mchungaji kuomba msaada, atamuuliza “ unaenda wapi kwani huna kwenu?”. Hata akijieleza kuwa kaenda ili kupata ushauri, maana wanaweza mvumilia kwa siku chache hata kama watampa hifadhi ila baada ya muda mfupi watamuuliza kwanini haendi kwao kama kafukuzwa na mume wake? Maana hatakiwi kukaa tena kwa mchungaji wake.

Kwa hiyo Biblia inatuambia kuwa wanawake wanatakiwa wawe na akili za kuwapenda waume zao na kufanya kazi nyumbani  mwao ili neno la Bwana lisitukanwe. Pia kwa wanaume wanatakiwa wawe na akili za kuishi na wake zao vizuri ili kuomba kwao kusizuiliwe. (Kesho tutaangalia uhusiano wa akili na imani.)


*MFANO WA TANO.*
*V. UBONGO UNATAKIWA UKUSAIDIE KUWA NA MIPANGO YA KUPATA PESA LAKINI AKILI INATAKIWA ZIKUSAIDIE KUAMUA JUU YA CHANZO CHA KUPATA PESA NA KUAMUA MATUMIZI YA PESA HIZO*

*Waebrania 5:14*
_“Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao

akili zao, kwa kutumiwa, zimezoeshwa kupambanua mema na mabaya.”_

Kazi mojawapo ya akili ni kutusaidia kupambanua mema na mabaya kwa jinsi ya Ki-Mungu ili tuweze kuchagua mema na kuacha mabaya. Biblia inatuambia kuwa *akili zao kwa kutumiwa.* haijasema kwa kutegemewa bali ni kutumiwa. Biblia imekataza kutegemea akili bali tunatakiwa tumtegemee Mungu.

Shetani akitaka kuvuruga maisha yako atakamata akili zako maana ubongo unaweza kuwa na mipango mizuri sana ya kupata pesa lakini akili zako zisiwe vizuri katika kuangalia chanzo na matumizi ya pesa zako. Maana unaweza ukawa na mipango mizuri sana mbele ya watu au nchi lakini inaweza isikupe hela. Maana unaweza pata hasa sadaka ya shukrani ya kutoa jumapili katika hizo pesa zako.  Lakini chanzo chako hakiko sawa maana kumbe hizo pesa umevunja benki mahali ukaiba.

Fikiria  mtu ambaye kaenda shule vizuri na kawa mhasibu mzuri na anapata mshahara mkubwa sana. Kitu cha kwanza anachofanya akiwa kazini anaanza kuiba. Sasa hapo kapata kazi kwa kutumia ubongo lakini akili zake haziko kazini na kwa sababu hiyo shetani anazitumia kumfanya aibe. Maana kama kaenda chuo na kapata cheti kwamba kasomea masuala ya accounting na Finance. Sasa badala ya kwamba kwa kuwa kasoma vizuri basi atumie ujuzi wake kuandika vizuri katika kutunza kumbu kumbu vizuri yeye anaandika asionekane kama kaiba pesa kumbe anaibia shirika au kampuni anayofanyia kazi.

Lakini watu wa  namna hii wanasema ni wizi wa kutumia akili. Lakini akili zimetumika vibaya na kumfanya mtu kwenda kuiba. Unahitaji kuwa na akili nzuri ambazo zinakuelekeleza kuwa hii njia ni sahihi lakini hii ni mbaya.

Akili inakusaidia juu ya kutumia pesa  hasa katika kuweka akiba.

*Mwanzo 41: 33-36*
_*Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri.* Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa._

Yusufu alimwambia Farao atafute mtu wa akili na hekima ili akae juu ya Misri aweze kuweka akiba kwa ajili ya kipindi cha njaa.

*Mithali  30: 24-25*
_Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo; Lakini vina akili nyingi sana.   Chungu ni watu wasio na nguvu; Lakini hujiwekea chakula wakati wa joto._

Chungu ni watu wasio na nguvu, sasa haina maana hawa ni watu ila inapofika katika suala la kuweka akiba wana akili kama za watu. Lakini ukweli ni kuwa chungu ni aina ya siafu au sisimizi. Katika ;

*Mithali 6:6-11*
_Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima.  Kwa maana yeye hana kiongozi, Wala msimamizi, wala mkuu,  Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.  Ewe mvivu, utalala hadi lini? Utaondoka lini katika usingizi wako?   Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi!Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha._

Kuna umasikini wa kukosa akiba na si umasikini wa kukosa pesa maana  watu wengi ndio wamekwama hapa. Shida yake iko kwenye akili maana Mungu kaweka akili ifanye maamuzi ya kuweka akiba. Sisimizi huwa wanakusanya chakula wakati wa hari/kiangazi ili kitumike wakati wa baridi.

Kama hujakaa nchi za baridi unaweza usielewe maana unaweza fikiria baridi kama ile ya mwezi wa sita tu.Sasa ile baridi kwa msemo wa mjini tungesema hiyo ni cha mtoto. Sasa ukienda nchi za Kaskazini au kusini mwa dunia. Kuna baridi kali sana huwa inaanza mwezi October hadi Machi. Kunakuwa na baridi kali sana maana huoni hata sehemu ya ardhi hasa kama unapita na ndege isipokuwa barabara tu ambapo huwa wanakwangua.

Baridi inashusha barafu sana maana inaweza shusha hadi dari ya nyumba maana ni nzito sana. Maana hata gari likiachwa nje huwa linafunikwa na barafu kabisa hadi kesho unaweza usilione maana linakuwa limefunikwa kabisa. Maana huwa wanachimba n

a spedi ili kuweza kulitoa gari lilipofunikwa na barafu.

Sasa unaweza ukaelewa hawa wadudu wanakaa kipindi chote cha baridi wakiwa hai. kwa hiyo wanajua kuna kipindi cha kukusanya, maana wanajua kabisa hawatakiwi kula chakula chote maana wanajua kuna msimu wa njaa. Biblia inaposema hawana akida maana yake hakuna mtu wa kuwasimamia au hawana serikali ya kuilalamikia kuwa wanapita kipindi cha njaa kwa hiyo wanahitaji msaada. Wasipoweka akiba ni kwa hasara yao maana ukifika wakati wa baridi watakosa chakula na mwishowe watakufa.

Watu wengi ambao hawana akiba sio kwamba  hawana hela bali ni kuwa hawajui mgawanyo  na kinachogawanya pesa za sasa na za kesho ni akili, sio roho. Ukitaka kukwama sasa hapo jaribu kwenda kiroho kuweka akiba, ujue lazima utakwama tu.

*USHUHUDA.*
Kuna rafiki yetu mmoja alikuwa anakula kila kitu anachopata. Alikuwa anasema siweki akiba maana sitaacha mtu hapa Duniani. Kwa hiyo alikuwa akipata kila chochote anakula kila kitu hata hatunzi akiba maana alikuwa anasema wasije watu wakagombania siku tukifa maana itakuwa shida sana. Kwa hiyo hata kama kapata zaidi basi kilichozidi alikuwa anatoa sadaka. Siku moja walipata ajali yeye na mke na watoto wao wawili wote walikufa.

Huyu ndugu japo walikufa wote siku moja yaani yeye na familia yake lakini alikuwa  anaishi kiroho, lakini haitakiwi uishi hivyo maana lazima ujue kuna kesho, kuna watoto watabaki  kwa hiyo tumia akili yako vizuri kuweka akiba.

Pia katika kuweka akiba weka akiba kwa utaratibu ambao Mungu kakupa.Wamisri walipoambiwa waweke akiba ya nafaka wao waliweka akiba za pesa na za wanyama. Sasa akiba yao iliishia baada  ya muda mfupi na haikuwa na msaada kwao maana baada ya mwaka mmoja walimaliza kika kitu. Walijiuza wao na ardhi yao na haikuwa wakiwatosha. Maana  bado walikuwa na miaka minne mbele na hawana kitu.

Tuje kwako wewe je akiba ambayo unayo kama iko benki au mahali popote unapojua wewe, jaribu kufikiria  kama huna kipato chochote kuanzia sasa na huna msaada wowote, je hiyo hela uliyonayo itakufikisha wapi? Ndipo  utagundua kuwa  hata mwezi humalizi ndipo utajua maisha yako yako hatarini kiasi gani. Biblia inaita umasikini wa kukosa akiba maana sio umasikini wa kukosa kipato.

Shetani akitaka kukubana  ili ukose akiba, atabana fikra zako wakati wa kiangazi ili usiweze kuweka akiba. Atabana akili zako uko kazini wakati huo unapata mshahara wako vizuri na unafikiri kuwa hiyo kazi haitaisha na hata wewe hukumbuki kuweka  akiba. Atabana wakati biashara yako inaenda vizuri ili usikumbuke kuweka akiba wakati biashara inaingiza pesa nyingi, wewe hukumbuki hata kuweka akiba maana unajua huo mzunguko utakuwepo na kesho.

Kumbuka kuwa kuna kipindi cha miaka saba ambacho  kinaweza kikaja na shida, lakini wakati wa unono wa miaka saba unabanwa hata hukumbuki  kuna kipindi cha njaa kinakuja. Hapo ndipo shetani anabana watu wengi sana maana unakuwa na pesa lakini unabanwa kuweka akiba. Hata ukijaribu kudunduliza unakwama kabisa. Shetani akitaka kukubana  atakubana wakati una kipato kizuri usiweke akiba kwa ajili  ya wakati ambao hutakuwa na kipato hicho tena.

Maana akili zako zinakuwa zimebanwa kabisa unapata pesa na unazitumia kienyeji kienyeji tu. Ili uweze kuelewa tafuta watu waliostaafu. Wengi sana wana maisha mabaya na ni wachache sana wana maisha mazuri, kwa sababu wengine walikuwa  na maisha mazuri sana walipokuwa kazini.  Walikuwa na magari na nyumba kumbe ni za shirika au kampuni ambayo anafanyia kazi lakini sio vya kwake. Maana wakati wa zamani  wafanyakazi walikuwa wanapewa kila kitu hadi furniture za ndani, ukiwaona utafikiri ni vya kwao kumbe sio vyao ni vya shirika akifukuzwa kazi au hiyo kazi ikiisha ndipo utaona namna maisha yake yanavyobadilika kabisa.

Tulikuwa mkoa mmoja, tulikuta mchungaji ambaye alifariki ghafla akiwa kwenye safari ya kikazi. Aliacha watoto wake sita, mke wake na watoto wa ndugu zake sita. Kwa hiyo nyumbani kwake kulikuwa na watoto kumi na mbili.

Mchungaji mpaka anakufa alikuwa hana nyumba. Baada ya mazishi na baada ya miezi mitatu kupita wazee wa kanisa na baadhi ya Viongozi wa lile kanisa wakimwendea yu

le mke wa mchungaji aliyefariki.Wakamuambia  kuwa mama tunamshukuru Mungu kwa ajili yamume wako maana  kwa kweli tuliona mkono wa Mungu juu yake sijui kwanini Mungu alimchukua mapema.

Walianza mbali kuanza kuongea nae, na walisema mama unajua kilichotuleta ni kuwa mambo lazima yaende na Mungu katupatia mchungaji mwingine. Sasa tunahitaji hii nyumba ili aje aishi hapa. Yule mama alikuwa hana mahali pengine pa kwenda yule mama alitusimulia yeye mwenyewe maana anasema baada ya hapo alianza kulia na akapata pressure na akaugua muda mrefu sana. Ile kazi aliyokuwa anafanya  alifukuzwa maana hakuonekana kazini muda mrefu sana kwa sababu ya kuumwa.

Je unataka kwenda kiroho na future ya familia????, unakufa hujaacha mambo ya familia kikaa sawa,  ukiondoka unawachia mama na watoto mzigo mzito sana.

Wimbo.. Nina haja nawe….


11. NINA HAJA NAWE

Nina haja nawe
Kila saa;
Hawezi mwingine
Kunifaa.

    Yesu, nakuhitaji
    Vivyo kila saa!
    Niwezeshe, Mwokozi,
    Nakujia.

Nina haja nawe;
Kaa nami,
Na maonjo haya,
Hayaumi.

Nina haja nawe;
Kila hali,
Maisha ni bure,
Uli mbali.

Nina haja nawe,
Nifundishe
Na ahadi zako
Zifikishe.

Nina haja nawe,
Mweza yote,
Ni wako kabisa
Siku zote.

                  *BARIKIWA SANA NA BWANA*

Post a Comment

0 Comments