1⃣ SEMINA YA NENO LA MUNGU KWA WATU WOTE - MOSHI - UWANJA WA MPIRA MAJENGO

   Na _MWL._
                        CHRISTOPHER
                                          MWAKASEGE

SOMO: NAMNA YA KUSHINDA VIKWAZO VINAVYOZUIA USIFIKIE MALENGO YAKO KIMAISHA.

TAREHE:  25 /02/ 2019

SIKU YA KWANZA

UTANGULIZI

Somo nililonalo kwa semina yetu hii lina kichwa kinachosema *NAMNA YA KUSHINDA VIKWAZO VINAVYOZUIA USIFIKIE MALENGO YAKO KIMAISHA.* Ni somo la muhimu sana ambalo linatakiwa nifundishe kwa mtu mmoja mmoja upate kuuliza na maswali lakini Roho Mtakatifu yuko pamoja nasi ili apate kusema na kila mmoja peke na utauliza maswali rohoni mwako naye Roho Mtakatifu atakupa majibu hapo hapo.

Kuna mambo makuu makubwa mawili tutakutana nayo kwenye hili somo ambayo ni vikwazo au vizuizi vinavyosababisha usifikie malengo yako kimaisha.

*KIKWAZO CHA KWANZA*

*A. AKILI KUFUNGWA NA SHETANI.*
*Luka 8:26 - 39*
_“Wakafika pwani ya nchi ya Wagerasi, inayoelekea Galilaya. Naye aliposhuka pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule, mwenye pepo, hakuvaa nguo siku nyingi, wala hakukaa nyumbani, ila makaburini. Alipomwona Yesu alipiga kelele, akaanguka mbele yake, akasema kwa sauti kuu, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakusihi usinitese. Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo. Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia. Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni. Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa. Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji. Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka kwenda kuliona lililotokea, wakamwendea Yesu, wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi miguuni pa Yesu, amevaa nguo, *ana akili zake;* wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza jinsi alivyoponywa yule aliyepagawa na pepo. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi. Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema, Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu.”_

Tunataka kuangalia hiki kikwazo cha akili kufungwa katika malengo ya maisha ya mtu. Tunamwona huyu mtu akili zake zilifungwa ingawa mapepo yalikuwa mengi sana juu yake lakini mapepo hayo yalilenga kushika na kufunga akili zake ili zisifanye kazi inayotakiwa na aliishi kama mtu asiye na akili kabisa .

Ili tuliangalie hiki kikwazo kuna mambo kadhaa tunapaswa tufahamu kwa undani kuhusu akili ili upate kuelewa kama umekwama hapo Mungu aweze kukufungua.

JAMBO LA KWANZA.
*1. MTU NI ROHO, ANAYO NAFSI ANAKAA NDANI YA MWILI.*
*2 Wakorintho 7:1*
_“Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.”_

Nataka tuone vitu vitatu hapo yaani NAFSI, ROHO NA MWILI.

Ukisoma pia
*Zaburi 42:5*
_*“Nafsi yangu,* kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.”_

Hapo anayesema “Nafsi yangu…” ni roho ya Daudi kwamba inataka kutuambia inayo nafsi na hiyo nafsi inakaa ndani yake. Kwa hiyo mtu ki roho anayo nafsi na anakaa ndani ya mwili.

JAMBO LA PILI
*2. ROHO YA MTU ILIUMBWA KWANZA HALAFU UKAUMBWA MWILI NDIPO NAFSI IKAUMBWA.*
*Mwanzo 2:7*
_“BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”_

*Mwanzo 1:27*
_“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.”_

Sura ya pili inatuambia hakukuwa na mtu wa kuilima ardhi kwa hiyo Mungu hakuinyeshea mvua ardhi. Sura ya kwanza inasema Mungu alimuumba mtu kwa

mfano wake mwanamume na mwanamke aliwaumba.

Lazima uzisome hizi sura mbili kwa pamoja kila sura kwa wakati mmoja maana ukisoma moja moja zitakusumbua kwenye uumbaji. Maana ukitaka kufahamu jinsi uumbaji ulivyoenda sawa ni lazima usome hizi sura zote mbili kwa pamoja maana zinaenda pamoja
Sura ya kwanza Mungu alimuumba mtu roho, yaani roho yake ndipo ilipoumbwa, aliumba kwa mfano wake mwanamume na mwanamke wote roho zao ziliumbwa sura ya kwanza.
Sura ya pili unaona vitu vyote vilivyokuwa vikitamkwa kwenye sura ya kwanza huvioni. Hakukuwa na mche wowote kondeni wakati kule mwanzo kulikuwa na miti na kila kitu vizae na alizungumza juu ya wanyama, ndege na n.k lakini kwenye sura ya pili huvioni unaona vyote vinatoka kwenye udongo. Alikuwa anatengeneza miili yao. Maana mtu alipoumbwa mwanzoni walipewa mwili mmoja mwanamume na mwanamke waliishi kwenye mwili mmoja.
*Mwanzo 5:1-2*
_“Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya; mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa.”_

Wote walipewa jina moja Adamu, na alipokuwa anaumba hakusema anaumba watu bali alisema anaumba mtu na ina sababu zake.

*Mwanzo 2:7*
_“Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”_

Kwa hiyo unaona nafsi ikitamkwa kwa mara ya kwanza hapa. Maana yake ni kwamba nafsi ilifuata ya tatu, roho iliumbwa kwanza ikafuata mwili na nafsi ndipo ikamalizia. Ni muhimu sana uweze kufahamu hizi katika mpangilio wake.

JAMBO LA TATU
*3. NAFSI NA MWILI VILIUMBWA VIMILIKIWE NA ROHO*

*Zaburi 63:1*
_“Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.”_

Mwandishi anamwambia Mungu, “Mungu wangu nitakutafuta mapema”, anaposema *nitakutafuta* ni roho ya Daudi inamweleza Mungu ya kwamba nitakutafuta mapema.

Roho hiyo hiyo inasema kwa niaba ya nafsi, inasema nafsi yangu inakuonea kiu, lakini pia inasema kwa niaba ya mwili inasema mwili wangu wakuonea shauku.

Nilitaka uone ya kwamba hauwezi kusema nafsi yangu kama haijapangiwa imilikiwe na roho na hauwezi kusema mwili wangu kama roho haikupangiwa kumiliki mwili.

Ni dhambi iliyokuja na kukorofisha utaratibu wa uumbaji na mwili ukaonekana kama ndio unao tawala kila kitu, lakini Mungu aliweka kwa makusudi kabisa kwamba roho ya mtu ndiyo imiliki nafsi na mwili.

JAMBO LA NNE
*4. AKILI IMO NDANI YA NAFSI*

*Ayubu 32:8*
_“Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.”_

Unganisha na kile kitabu cha Mwanzo ili uelewe vizuri zaidi:

*Mwanzo 2:7*
_“Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”_

Kwa hiyo kama pumzi iliachilia nafsi ndani ya mtu na pumzi iliachilia akili ndani ya mtu kwa hiyo akili imo ndani ya nafsi.

Akili tumeipata kwa msaada wa pumzi ya Mungu na nafsi tumeipata kwa msaada wa pumzi ya Mungu. Wakati nafsi inaingizwa ndani yetu na akili ziliingizwa, na ndiyo maana kama unayo nafsi lazima na akili unazo, hakuna mtu ambaye ameumbwa bila akili, ile kwamba huzitumii haina maana kwamba huna.

JAMBO LA TANO
*5. AKILI SIO UBONGO, LAKINI MUNGU ALIVIUMBA VIFANYE KAZI KWA KUSHIRIKIANA*

Biblia ya Kiswahili inafundisha vizuri zaidi juu ya akili kuliko Biblia ya Kiingereza. Ukisoma Biblia ya Kiingereza unahitaji kuwa mwangalifu sana kutafuta neno akili kwa sababu limeandikwa kwa tafsiri tofauti tofauti kutegemeana na waliokuwa wakitafsiri na inategemea pia picha nzima ya habari inayozungumzwa.

Kwa sababu ubongo kwenye Kiingereza wanasema ni *Brain* lakini wengine wanasema ni *Brains* wengine wanasema ni *intelligence* na wengine wanasema ni *mind* lakini kwenye Biblia ya Kiswahili wamenyooka na kupata neno nzuri kabisa ambalo ni akili.

Ubongo upo kwenye mwili na akili ipo kwenye nafsi. Na ndiyo maana hata ukienda hospitali wataalam watakuambia ubongo ulipo lakini watapata shida sana kukueleza akili zilipo.

Mungu aliumba akili na ubongo vifanye kazi pamoja lakini akili imo ndani ya na

fsi na ubongo umo ndani ya mwili.

Kazi ya ubongo ni *kupokea elimu* na kazi ya akili ni *kuchukua elimu na kuibadilisha kuwa maarifa* Ubongo haubadilishagi elimu kuwa maarifa.

Na ndiyo maana ukishikwa akili zako hata kama una akili kiasi gani ubongo unaweza kukusaidia ukafaulu darasani lakini huwezi kufaulu kwenye maisha. Kwa sababu maisha hayafaulishwi na ubongo wako bali ufaulishwa na akili yako na nafsi yako.

Biblia inasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa na sio kwa kukosa ubongo. Na ndiyo maana mtu anaweza kuwa na shahada kadhaa lakini maisha hana. Ile tu kwamba mtu amesoma haina maana kisomo kinampa maisha. Kisomo kinaweza kikakupa cheti, kazi, heshima kwenye jamii lakini hakiwezi kikakupa maisha kwa sababu maisha yalinyang’anywa dhambi ilipoingia maana mwanadamu hakupewa maisha ya kwake alipewa maisha ya Mungu ambayo yanaitwa uzima. Yesu alisema nimekuja ili wawe na uzima kisha wawe nao tele. Huwezi kupata maisha ambayo Mungu aliyakusudia nje ya Yesu.

Ubongo unapokea *habari/information* lakini akili *inageuza habari kuwa ufahamu*

Haisemi ndipo akawafunulia akili zao wapate kusoma maandiko, kusoma hakuna shida, unaweza kusoma Biblia, ukakariri na kuimaliza yote lakini kuielewa akili lazima iingie kazini.

*1 Petro 2:1-2*
_“Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;”_

Hakusema maziwa ya Roho amesema maziwa ya akili, Neno la Mungu unalopewa unapookoka mahali pa kushughulika napo pa kwanza ni akili zako ili upate kuukulia wokovu, ndio maana akili zikibanwa haijalishi umeokoka miaka mingapi huwezi kukua kiroho, ndio maana huwezi kujivunia miaka uliyokaa ndani ya wokovu, Mungu anaangalia umekua kiasi gani na usipojua kwamba Mungu kaziweka akili kwa makusudi kabisa macho na ubongo vitakusaidia kusoma Biblia lakini haviwezi vikakusaidia kuelewa.

*Mathayo 7:24*
_“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”_

Huyu ni Yesu anazungumza anasema mtendaji wa Neno amefaninishwa na mtu mwenye akili hajasema amefananishwa na wa kiroho.

Watu wengi sana hawajui namna ya kuunganisha akili na imani, wanafikiri mtu aliyeokoka akitumia akili anaenda kimwili na sasa umeelewa kwamba akili haziko kwenye mwili, Biblia imekataza tusizitegemee akili lakini tuzitumie akili.

Yule mtu ambaye alikuwa na kichaa alipofunguliwa yale mapepo wale watu kwenye kijiji walikuja kumtazama pamoja nakumwona amevaa nguo na ana utulivu wakagundua ana akili zake. Maana yake walitambua ya kwamba huyu mtu maisha aliyokuwa anaishi akili hazikuwa kazini.

Ukisoma hiyo mistari vizuri kwa jicho la mwalimu kuna kitu hapo utaona
*Luka 8:22,37*
_“Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi.”_

Roho Mtakatifu alimbana Yesu wakati huduma ilikuwa inaendelea ukitazama pale aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha kwa maana walimgojea wote utafikiri aliwaambia kuna jambo naenda kuangalia narudi sasa hivi, maana aliporudi tena ng’ambo mkutano mkubwa ulikuwa unamgojea.

Yule mtu Biblia haituambii jina lake lakini mbingu zilikuwa zinamfahamu na maandiko yanatuambia alikuwa na kwao kwa sababu alipotaka kumfuata akamwambia nenda rudi nyumbani kwako.

Inawezekana alikuwa na wazazi, alikuwa na ndugu alikuwa na majirani, alikuwa pia na marafiki lakini mazingira yalimbana kiasi kwamba akawa anashinda makaburini na milimani na maandiko yana

sema kuna kipindi ilibidi afungwe ili kuweza kuhimili ile vurugu ambayo alikuwa anafanya.

Inawezekana wote walimkatia tamaa na yale mapepo yalikuwa ndani ya mtu na yalikuwa yanamkwamisha yeye mwenyewe maana anakimbilia kufanya vitu na yanamkwamisha. Maana tunaona mapepo baada ya kutoka yaliingia ndani ya nguruwe na kuwapeleka majini kwa kasi. Sasa haya mapepo ndio yalikuwa ndani ya mtu yakimsukumia wazo la kufanya na kinamharibu na kumwamisha jumla kabisa.

Hii unaweza ukasikia mtu akisema _“nimemlea huyu mtoto nikifikiri akili anazo kumbe hana”._ Ukishasikia lugha ya nmna hiyo ina maana akili hazifanyi kazi inayotakiwa kwa sababu hamna mtu ambaye hana akili ila kuna namna zimebanwa.

Sasa angalia yule kijana wa nchi ya Wagerasi kila mtu alikuwa kamkatia tamaa. Sasa Yesu alikuwa hafanyi jambo lolote isipokuwa kamuomba baba akifanya. Kwa hiyo walikuwa anafanya mapenzi yake maana alikuwa akimuona Yesu kayakamilisha. Yesu aliposema tuvuke mpaka ng’ambo ina maana aliuacha mkutano mkubwa alafu akaingia katika boti kwenda ng’ambo mpaka nchi ya Wagerasi.  Wanafunzi wake walikuwa hawajui wanaenda kufanya nini huko lakini Roho Mtakatifu alikuwa anajua kwamba kuna mtu yupo makaburini hapati hata msaada maana tunaona hakupelekwa na watu kwa Yesu.

Maandiko yanatuambia kuwa Yesu alipofika tu alianza kukemea mapepo  na ndio maana yalianza kupiga kelele kuwa tuna nini na wewe Yesu. Yesu alimfuatilia yule kijana maana tunaona hamna mtu aliyempeleka kwa Yesu kwa sababu kulikuwa na mkutano ng’ambo ya ziwa kwa sababu wangekuwa na haja ya kumpeleka wangempeleka kwa Yesu alipokuwa ng’ambo maana boti zilikuwepo za kuweza kuwavusha hata ng’ambo ya pili. Kila mtu alikuwa amemuacha na hapati msaada hata ndugu zake hawakumsaidia.

Unisikilize inawezekana kabisa uko mahali na kila kitu chako kimekwama, nipo hapa kukuambia neno la Bwana  kuwa Yesu yupo ng’ambo na atakuja kukufuata na wewe ili aje kukutembelea.  Haijalishi maisha yako yako mahali pagumu kiasi gani kama vile makaburini  Yesu atakuja yeye mwenyewe kukufuata hata kama haujakaribishwa kwenye mkutano.

Yesu alipomfuata yule kijana alihusika moja kwa moja na akili zake maana alijua kabisa ya kwamba yule kijana akifunguliwa akili tu anaweza akasimama peke yake. Yule kijana alipoponywa biblia inatuambia alivaa nguo. Sasa swali linakuja hizo nguo alizipata wapi? Kwa hiyo  inawezekana kabisa hakuchana nguo zote bali alikuwa anavua kila akivalishwa. Maana hatuoni kama kuna mtu alimpa nguo hata watu wa pale  maana  hata Yesu mwenyewe hakuja na nguo wala wanafunzi wake  za kumpa yule kijana.

Biblia inatuambia kuwa wanakijiji walipokuja walimkuta tayari kavaa nguo. Wafugaji wa pale walioopona nguruwe wamejimwaga baharini  walikimbia mtaani kuwaeleza watu. Sasa yule kijana akili zake ziliporudi alitafuta nguo zake. Sasa akili zikifanya kazi jamii itakupa heshima hata kama haitaki. Biblia inatuambia kuwa walipokuja walimkuta yule kijana aliyekuwa na pepo kavaa nguo zake na katulia pale na akili zake zikiwa vizuri waliogopa sana. Baada ya hapo walimuomba Yesu aondoke kwao, na Yesu alitii aliondoka akapanda boti na akarudi kwenye mkutano.

Mungu anaweza akaleta  semina hii kwa ajili yako tu. Kwa hiyo isikusumbue umati wa watu bali angalia kama Yesu amekutembelea  au hajakutembelea. Kuna watu kwenye biblia  tunaona watu waliokuwa wanaleta wagonjwa kwa Yesu ili wapate msaada  lakini yule kijana wa nchi ya Wagerasi hakuna aliyempeleka kwa Yesu. Labda inawezekana watu walimuogopa kwa sababu alikuwa mgomvi na ana mapepo.

Sasa inawezekana  kuna mtu wa namna hiyo nyumbani kwenu ambaye mnasema mtu huyu anakua mwili tu ila akili hamna na mnamkalia na kikao kabisa kwa ajili yake maana mna wasi wasi na akili zake. Kuna watu wengi sana ambao shetani kabana akili zao na za ndugu zao maana shetani hafungi mwili tu bali anafunga na akili pia. Shetani anaweza akalenga kufunga akili zenyewe kwa sababu ya umuhimu wake kwa sababu atakuwa ameshika sehemu kubwa sana ya akili yake na anakwamisha maisha yake.

Kuna mtu unakuta kasoma vizuri sana na ana degree mbili hivi au tatu. Anaanza kazi vizuri kabisa lakini baad

a ya muda anaacha. Ukimwuliza kwanini atakuambia kuwa huku kazini wananisumbua sumbua tu. Sasa unamwuliza sasa utafanya nini sasa anasema nitafanya biashara.  Hapo mtaji hana, hana hata uzoefu wa biashara, kakaa tu hapo nyumbani ila anasema nitafanya biashara. Baada ya hapo utamuona anaanza kuingia kwenye vijiwe na kukaa na watu huko. Hii ni kwa sababu akili zinafanana na anao kaa nao maana akili huwa zinaitana.

Biblia inasema aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo. Kwa hiyo kama unataka kubadili maisha yako tazama wanaokuzunguka. Kwa sababu kama wanafanana na wewe katika kufikiri. Kama unawapenda sana kaa nao mbali kwanza alafu alafu ukikaa sawa ndipo uje uwatoe kama gari iliyokwama kwenye matope.  Maana hamuwezi kusaidiana wote mkiwa kwenye matope,  Ondoka kwanza kwenye kijiwe katafute msaada kwa Yesu, na ukirudi ukiwa umebadikika ndipo  uje uwatoe kwenye kijiwe. Kwa sababu wataona namna kufikiri kwako na kuwaza kwako kulivyobadilika kwa sababu kuna kitu Mungu amefanya kwenye akili zako na zimefunguliwa.

Kijana wa nchi ya Wagerasi alipofunguliwa na akili zake kukaa sawa tunaona moto uliingia ndani yake na alitaka kumfuata Yesu saa hiyo hiyo. Alikuwa hajawaaga ndugu zake  na kwao lakini Yesu alimwambia rudi kwenu na waambie mambo makuu ambayo Yesu kakutendea. Maana yake akaanze ushuhuda nyumbani. Yesu akikutendea mambo makuu unakuwa na ushuhuda moto moto ambao unataka ukawaambie watu kumbe inatakiwa urudi nyumbani.

Wale Wafugaji walipata hasara maana yaliua nguruwe wao. Kwa hiyo lazima hawakuwa na habari nzuri ya Yesu kwa sababu mradi wao umekufa maana nguruwe walikuwa ni wengi walioingia majini ni zaidi ya nguruwe  2000.

Sema Mwakasege anamwaga zege……

Weka mikono yako juu ya kichwa ili tufanye maombi ambayo Mungu atafuatilia muunganiko wa ubongo wako na akili zako. Kama kuna mapepo katika akili zako yataachia tu kwa jina la Yesu.

Omba Mungu aponye akili zako na kuweka huo muunganiko vizuri kwa Damu ya Yesu.  Nyunyiza Damu ya Yesu juu yako.

Pia kama hujaokoka hakikisha unaokoka,  angalia link ya sala ya Toba na kitabu cha Hongera kwa kuokoka. Pia kama una ndugu yako unataka Mungu amponye akili zake andika jina lake tuma kwa namba za maombi tulizokuweka pale juu mwanzo wa somo hili.

Mungu akubariki sana.

Semina hii ni nzuri mno, jitahidi uisome, nunua CD/DVD ili uzidi kukua kiroho. Tuliopo Moshi ,Arusha,Tanga,Manyara, Kenya hakikisha huikosi

Post a Comment

1 Comments